Wawili kizimbani kwa kumzushia uongo Waziri Mkuu

Hakimu Mkazi Kisutu

0
225

Watu wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matatu ikiwemo la kuchapisha maudhui ya uongo dhidi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Washitakiwa Adam Thabiti na Heri Said wakazi wa Dar es Salaam wamefikishwa mahakamani hapo nakusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuge mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Evodia Kyaruzi.

Katika shitaka la kwanza washitakiwa hao mnamo Juni 20, 2021 wanadaiwa kusambaza ujumbe wa uongo kwamba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametumbuliwa wakati wakijua sio kweli.

Katika shitaka la pili wakili Katuge amedai washitakiwa hao wanadaiwa kuchapisha maudhui ya uongo dhidi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupitia You tube Channel inayoitwa Bongo News kosa ambalo wanadaiwa kulitenda Januari 2, 2021.

Aidha, katika shitaka la tatu washitakiwa hao wanadaiwa kuendesha chaneli ya mtandaoni bila kuwa na kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Hata hivyo washitakiwa wamekana kutenda makosa hayo na wameomba mahakama kuwapa dhamana kwa kuwa walipewa dhamana wakiwa chini ya Polisi, huku upande wa mashitaka ukiwasilisha hoja ya kuomba mahakama washitakiwa wasipewe dhamana kwa ajili usalama wao dhidi ya baadhi ya wananchi weneye hasira kali.

Hakimu Evodia ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 20, 2021 na washitakiwa wamerudishwa rumande.