Wakazi wa Dar kupata chanjo ya UVIKO-19 Jumapili

0
285

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema Jumapili wiki hii itakua siku maalum kwa wakazi wa mkoa huo kupata chanjo ya UVIKO-19 katika Uwanja vya Uhuru kwa hiari.

Amesema mchakato utawahusu wananchi wote wenye umri wa kuanzia miaka18 ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakikosa muda wa kwenda kupata huduma hiyo katika vituo vilivyoanishwa mkoani Dar es Salaam.

Makalla amewaambia waandishi wa habari kuwa chanjo hiyo itatolewa kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa 10 jioni.

Katika maelezo yake, amesema kwa nyakati tofauti amekuwa akipokea jumbe kwa njia ya simu na kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa wananchi wakimueleza kukosa huduma hiyo kutokana na majukumu yaliyowakabili hivyo kuamua kutenga siku ya Jumapili kwa ajili ya kutoa chanjo kwa watu wote.

Aidha amewaagiza wakuu wote wa wilaya kutenga siku moja katika wilaya zao kwa ajili ya wananchi wao kupata chanjo ya UVIKO-19.