TRA: Kodi ya majengo kwa LUKU haiwahusu wapangaji

0
516
Ulipaji wa kodi ya majengo kwa njia ya ununuzi wa umeme kuanza Agosti 20, 2021.

Serikali inaanza utekelezaji wa kukusanya kodi ya majengo kwa kutumia mfumo mpya wa ukusanyaji kupitia ununuzi wa umeme kuanzia Agosti 20, 2021.

Utaratibu huo utasimamiwa na Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Viwango hivyo kwa sasa ni shilingi 12,000 kwa kila jengo la kawaida ndani ya kiwanja kutoka shilingi 10,000 iliyokuwa ikitozwa awali, na shilingi 60,000 kwa kila sakafu ya ghorofa kutoka 50,000. Hata hivyo kwa upande wa halmashauri za wilaya na miji midogo nyumba za ghorofa bila kujali idadi ya sakafu zitatozwa shilingi 60,000.

Kwa utaratibu huo kila mnunuzi wa umeme atakatwa shilingi 1,000 kwa mwezi kwa nyumba ya kawaida na shilingi 5,000 kwa mwezi kwa kila sakafu ya ghorofa. Kwa wanaotumia mita za ankara watalipa kodi hiyo kwa pamoja katika Ankara zao za mwezi.

Akizungumza na TBC, Lazaro Lucas kutoka Kitengo cha Elimu kwa Umma, TRA amesema kuwa katika nyumba za wapangaji, mwenye nyumba atatakiwa kuwasilisha namba za mita za wapangaji ili wasikatwe kodi hiyo badala yake ilipwe na yeye mwenyewe.

“Hiyo kodi inapaswa kulipwa na mwenye jengo lakini kwa mwanzo kumekuwepo na changamoto ya kujua ni yupi mwenye jengo ni yupi mpangaji kwa hiyo mwanzoni [mpangaji] unaweza ukapata ‘bill’… mwenye jengo afike ofisini aseme nyumba zangu ni moja, mbili, tatu, ili wenye zile mita ziondolewe,” amesema Lucas.

Lucas ameongeza kuwa mwenye jengo anaweza kulipia kodi ya nyumba za wapangaji taslimu shilingi 12,000 kwa kila nyumba ya kawaida kwa mwaka na namba za mita za wapangaji zitaondolewa kwenye mfumo, au kodi hiyo itahamishiwa kwenye mita yake.

Aidha, TRA imesema kuwa endapo mwenye jengo hatowasilisha taarifa za wapangaji TRA, wapangaji wanaweza kupeleka malalamiko yao kwamba wanatozwa kodi ya jengo kimakosa.

Kuhusu udanganyifu wa idadi ya majengo, mamlaka hiyo imesema ni jukumu la mmiliki kusema idadi ya majengo yake, na endapo atadanganya, uhakiki ukifanyika atachukuliwa hatua za kisheria.

Wakati mfumo huu ukianza wale wote ambao nyumba zao hazina umeme wataendelea kulipa kodi kwa mfumo wa awali ambao ni njia ya simu ya mkononi au benki baada ya kupata namba ya kulipia (control number).