Serikali kuweka mashine za ukaguzi mizigo mipakani

0
138

Serikali ipo katika hatua za kuweka mashine maalumu za ukaguzi wa mizigo inayoingia na kutoka hapa nchini katika vituo na mipaka mbalimbali hapa nchini.

Naibu waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe ameyasema hayo leo alipotembelea kituo cha pamoja cha ushuru wa forodha mipakani (OSBP) kilichopo Namanga Mkoani Arusha akiwa ameambatana na Kamati ya kudumu ya Bunge ya bajeti.

Naibu waziri Kigahe amesema kuwa nia ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha inatatua changamoto zilizopo katika mipaka yetu ili kuchochea upatikanaji wa mapato na kurahisisha biashara.

“Serikali imekusudia kuweka vitendea kazi vya kupima magari makubwa (Scanner) na kudhibiti mizigo pamoja na kuondosha changamoto za msongamano wa magari na upimaji wa ugonjwa wa UVIKO 19” Amesema Mhe. Kigahe.

Aidha ameishukuru kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti kwa ushirikiano walioutoa kwa wizara ya viwanda na biashara hasa kutembelea miradi mbalimbali ya kimkakati na kutoa maoni yao ya kuboresha maeneo husika.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti Daniel Baran Sillo amesema kuwa uongozi wa wizara ya Viwanda na Biashara umetoa ushirikiano mkubwa kwa kamati anayoiongoza na waheshimiwa wabunge wamejionea na kusikiliza changamoto zote hivyo kamati yake itakaa na kufanya uchambuzi na kuishauri serikali namna bora ya kuboresha na kutatua changamoto zilizopo