Wafugaji kunufaika na mfumo mpya wa utambuzi wa mifugo

0
145

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameagiza kusimamishwa kwa zoezi la kuchanja Mifugo kwa njia ya uwekaji wa chapa kwenye mifugo katika mikoa ya Rukwa, Katavi, Tabora  na Kigoma ili kupisha zoezi la kutambua mifugo yote kwa mfumo wa Kielekroniki kwa kuvalisha hereni kwenye mifugo husika.
 
Ndaki ametoa maagizo hayo baada ya wafugaji kulalamikia zoezi la utambuzi wa mifugo kwa  kuwawekea chapa kwakuwa wafugaji huishia kutozwa tozo kubwa za chapa na maafisa mifugo.

Akizindua zoezi hilo wilayani Nkansi mkoani Rukwa, Waziri Ndaki amesema zoezi la kuvalisha hereni mifugo imelenga pia kupunguza vitendo vya kuibiana mifugo, kwakuwa hereni hiyo itakuwa imewekewa taarifa za kujitosheleza za mnyama na mmiliki wake halali na wala si vinginevyo.

Amesema kumekuwepo na matukio ya kuibiana mifugo matukio hayo yatapungua kupitia mfumo huo wa kuitambulisha mifugo kwa mfumo wa kielectroniki na kwamba Serikali itanufaika na mapato halali kupitia mfumo huo.

Baadhi ya wafugaji wa ng’ombe wilayani Nkansi wameeleza kufurahishwa na mfumo huo, kwani mifumo iliyokuwepo ilikuwa inawanufaisha maafisa ugani wa mifugo na wadau wengine wa mifugo badala ya kumnufaisha mfugaji na serikali.