Jeshi la polisi mkoani Mtwara limemkamata Jabiri Bakari kwa tuhuma za kujihusisha na uhalifu wa utekaji, ubakaji na kulawiti watoto katika wilaya ya Mtwara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mark Njera amewaambia waandishi wa habari kuwa mtuhumiwa huyo mwenye miaka 19 alikamatwa Agosti 12 mwaka huu maeneo ya Mbae, Manispaa ya Mtwara kufuatia msako uliofanywa na jeshi la polisi.
Kamanda Njera amesema kabla ya kukamatwa, mtuhumiwa aliwadanganya watoto wa kike watatu wenye umri wa miaka saba, nane na tisa ambao kwa nyakati tofauti aliwalaghai kwa njia mbalimbali na kufanikiwa kuondoka nao kwenda kwenye maeneo na kuanzisha makazi ya muda.
Amesema Juni 25 mwaka huu mtuhumiwa alimlaghai mtoto wa kike mwenye umri wa miaka saba eneo la Mbae Mashariki wilaya ya Mtwara wakati mtoto huyo akicheza na wenzake na baadaye akaondoka naye ambapo mtoto huyo alipatikana baada ya siku tano akiwa amefanyiwa vitendo vya ukatili.
Julai 8 eneo hilo hilo mtuhumiwa alimchukua tena mtoto wa kike mwingine mwenye miaka nane na kutoweka naye na kwenda kusikojulikana. Mtoto huyo alipatikana Julai 24 akiwa amefanyiwa vitendo vya kikatili.
Aidha, Agosti 6 mtuhumiwa alimchukua mtoto mwenye umri wa miaka tisa ambaye pia alipelekwa kusikojulikana na kufanyiwa vitendo vya ukatili. Kwa muhjibu wa Kamanda Njera, mtoto huyo alipatikana Agosti 7 kufuatia msako wa jeshi hilo.
Kamanda Njera ametoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wa Mtwara kuhakikisha ulinzi na usalama kwa watoto na kutambua watu wanaojihusisha na vitendo vya ukatili kwa watoto na kutoa taarifa.
