Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti yatembelea Taasisi za TEMDO na CAMARTEC

0
225

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imetembelea ya Taasisi ya Uhandisi na Usanifu wa Mitambo Tanzania (TEMDO) na Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) kujionea ugunduzi wanaoufanya pamoja na kufahamu mahitaji ya kibajeti ya Taasisi hizo muhimu kwa maendeleo ya Kilimo na Viwanda.

Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo iliambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe na kupata nafasi ya kupata taarifa za Taasisi hizo mbili na kukagua na kupata maelezo ya mashine, mitambo na ugunduzi uliofanywa na taasisi hizo zilizopo Chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Baada ya kutembelea Taasisi hizo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Daniel Sillo ameeleza kuwa Taasisi hicho zina umuhimu mkubwa sana katika mapinduzi ya Viwanda na Kilimo ili kufikia kilimo chenye tija kwa ajiri ya ukuaji wa Uchumi wa viwanda.

Vile vile, Daniel Sillo ameleza kuwa Kamati hiyo itakaa kwa Pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara pia Wizara ya Fedha na mipango ili kuona namna ya kusaidi ili kutatua changamoto zilizotolewa ili Taasisi hizo ziendelea kutekeleza majukumu yake vizuri.

Nae, Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa Taasisi hizo zikiimalishwa zina uwezo mkubwa sana na kazi ya Serikali ni kuziimalisha na kuzipa nguvu ya kutekeleza majukumu yake hivyo Wizara inaendelea kuzifanyia kazi changamoto zinazikumba Taasisi hizo.

Awali, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe ameeleza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara ina Taasisi 15 ikiwemo TEMDO na CAMARTEC, taasisi hizo zilianzishwa kwa makusudi ili kuendeleza Sekta ya Viwanda na Kilimo hasa katika kipindi hiki cha awamu ya sita ambacho Serikali imejipambanua katika uchumi wa viwanda.