Ujenzi Daraja la Tanzanite wafikia asilimia 91

0
205

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameipongeza TANROAD kwa usimamizi mzuri wa mradi wa ujenzi wa Daraja la Tanzanite, awali likifahamika kama Daraja la Selander.

Aidha, amepongeza kuhusishwa kwa wananchi na wakandarasi wengi wazawa huku akitoa maelekezo kuwa ni muda mwafaka sasa kuwepo na programu maalum ya kukuza na kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa ili fursa za kandarasi za ujenzi zinazoendelea hapa nchini baadaye ziweze kufanywa na wazawa.

Ameyasema hayo leo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo katika ziara iliyojumuisha wajumbe wote wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila ameeleza kuwa ujenzi huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 243.7 na sasa umefikia asilimia 91. Ameongeza kuwa asilimia 92 ya wafanyakazi katika mradi huo unaotarajiwa kukamilika Desemba 2021 ni wazawa.