Olympics: Washindi wa medali wa Uganda kulipwa mishahara

0
161

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amewazawadia wachezaji wa nchi hiyo walioshinda medali katika mashindano ya Tokyo Olympics 2020 yaliyofanyika kuanzia Julai 23 hadi Agosti 8, 2021.

Washindi wawili wa medali za dhahabu, Joshua Cheptegei na Peruth Chemutai wamezawadiwa magari aina ya Mitsubishi Outlander huku Jacob Kiplimo mwenye medali ya shaba akizawadiwa gari aina ya Mitsubishi L200.

Mbali na zawadi hizo Rais Museveni ameahidi kuwajengea nyumba washindi wote wa medali za dhahabu pamoja na wazazi wao huku washindi wote kwa pamoja wakiahidiwa zawadi ya donge nono la fedha taslimu.

Aidha, washindi wa medali za dhahabu, fedha na shaba watalipwa mishahara kwa mwezi yenye thamani shilingi milioni 5 (TZS milioni 3.2), milioni 3 (TZS milioni 2) na milioni 1 (TZS 649,161), mtawalia.

Kwa upande mwingine Botswana imewazawadia washindi wake sita medali za shaba kwenye mbio za kupokezana vijiti (relay game) kila mmoja nyumba ya vyumba viwili viwili.