Ulega ataka TAFICO kujiendesha kibiashara kufikia uchumi wa Bluu

0
218

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amelitaka Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kujipanga kibiashara pamoja na kiubia na makampuni binafsi ya uwekezaji mara baada ya kufufuliwa na kuzinduliwa rasmi ili liwe na tija kwa wavuvi na taifa kwa ujumla.

Ulega amesema hayo mara baada ya kufika katika ofisi za TAFICO zilizopo Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam na kufafanua kuwa ni lazima uwepo mkakati na mbinu za kujielekeza zaidi katika uchumi wa bluu ili nchi ifaidike na rasilimali samaki na mazao yake na kuhakikisha uchumi wa wavuvi wadogo unakua ili shirika hilo liwe na tija zaidi.

Ulega amemuelekeza Mwenyekiti wa Bodi ya TAFICO Prof. Yunus Mgaya kusimamia mbinu na mkakati imara wa ufufuaji wa shirika na kumpongeza kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa Prof. Mgaya ana uzoefu mkubwa kwenye sekta ya uvuvi na kwamba ataweka dira imara ya TAFICO katika mikakati ya kuhakikisha shirika linakuwa na tija kwenye sekta ya uvuvi hususan katika uvuvi wa bahari kuu.

“Hivi karibuni haitazidi miezi mitatu tunapokea meli ya uvuvi tunataka ikifika ianze kazi mara moja, meli ikute tumekaa kwenye mpango kazi iende kuvua samaki wa kutosha bahari kuu na ilete hao samaki kwa wingi wauzwe ndani na nje ya nchi.” Amefafanua Ulega

Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa TAFICO Esther Mndeme amesema ukarabati unaendelea kufanywa katika miundombinu mbalimbali iliyopo kwenye eneo hilo baada ya serikali kufufua shirika hilo na kwamba baadhi ya miundombinu inahitaji ukarabati mkubwa na mingine kidogo kutokana na miundombinu hiyo kutofanya kazi kwa takriban miaka ishirini.

Mndeme amesema licha ya changamoto za kifedha Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha ukarabati huo unafanyika kwa muda uliopangwa ili shirika lianze majukumu yake rasmi kama ambavyo imekusudiwa.