Wanaopangisha nyumba za Serikali kinyemela kukiona

0
170

Shirika la Nyumba la Taifa mkoani Kilimanjaro, limewataka wapangaji wake kuacha tabia ya kupangisha watu wengine kinyemela katika nyumba zao kwani kufanya hivyo ni ukiukwaji wa kanuni na sheria za shirika hilo.

Akizungumza na TBC, Meneja wa Shirika hilo mkoa wa Kilimanjaro Juma Kiaramba amesema wapo baadhi ya wapangaji wamekuwa na tabia ya kupangishia watu wengine huku wakifahamu kuwa ni ukiukwaji wa sheria.

Kiaramba amewataka waliopangishwa nyumba isivyo kihalali, kujitokeza katika ofisi za Shirika la Nyumba ili hatua ziweze kuchukuliwa kwani kutokufanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

Baadhi ya wapangaji wa Shirika la nyumba mkoa wa Kilimanjaro wamesema kitendo cha baadhi ya wapangaji kupangisha watu wengine ni kulihujumu shirika hilo.

Wapangaji hao wamesema pia hali hiyo inamnyima haki zake za kimsingi mpangaji aliyepangishwa kinyemela pindi anapopata changamoto yoyote kwenye nyumba aliyopangishwa.

Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021, Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kilimanjaro limekusanya kiasi cha shilingi Bilioni 2.8 kutoka kwa wapangaji wake sawa na asilimia 100.

Sauda Shimbo- Moshi