Polisi DRC wapambana na waandamanaji

0
1196

Polisi wa kutuliza ghasia mjini Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wamepambana na waandamanaji waliokuwa wakipinga tangazo la serikali la kuzuia kampeni za uchaguzi mjini humo.

Wafuasi wa mgombea wa upinzani Martin Fayulu wamepambana na polisi baada ya kukiuka amri ya serikali ya kuzuia mikusanyiko ya kisiasa mjini Kinshasa, kwa madai kuwa inaweza kuleta ghasia, huku waandamanaji hao wakisema kuwa wananyimwa haki yao ya msingi.

Fayulu ameelezea kusikitishwa na amri hiyo ya serikali na kusema kuwa atakutana na uongozi wa Tume ya Uchaguzi katika Jamhuri hiyo ili kuhoji ni kwa nini imetolewa mara baada ya yeye kutangaza nia yake ya kuanza kampeni.

Uchaguzi mkuu wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo unatarajiwa kufanyika Jumapili ijayo na Fayulu amewalalamikia askari wa Jamhuri hiyo kwa kuwarushia risasi za moto wafuasi wake katika miji ya Kalembu na Lubumbashi ambako nako amezuiwa kufanya kampeni.

Serikali ya DRC ilitangaza kuwa huenda zoezi la kupiga kura nchini humo likachelewa kuanza siku hiyo ya Jumapili kutokana na sababu za kiufundi.

Karibu vifaa vyote vya kupigia kura viliteketezwa kwa moto katika ghala la kuhifadhia vifaa hivyo mjini Kinshasa wiki iliyopita, lakini serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ikatangaza kuwa uchaguzi huo  utafanyika kama ulivyopangwa.