Waliochanjwa kupewa vyeti vya kielektroniki

0
173

Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeeleza kuwa inaendelea na utaratibu kwa kuandaa mfumo wa kielektroniki wa vyeti vya chanjo dhidi ya UVIKO-19 (COVID-19 Vaccine Electronics Certificates), vitakavyokidhi vigezo vya kimataifa ikiwa ni kuhakikisha taarifa za wote waliochanjwa zinakuwa salama.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi na ameeleza kuwa vyeti hivyo vipya vitakuwa na taarifa zote za mhusika ikiwa ni pamoja na aina ya chanjo, sehemu na muda aliochanjwa, na amewaonya wale wote wanatakaojaribu kupata vyeti kwa njia ya udanganyifu.

“Ikumbukwe kuwa, wizara inafahamu mfuatano wa namba zake na zimetolewa kituo gani hivyo, ikitokea namba moja imejirudia uchunguzi utaanzia kwa watoa huduma waliotoa namba hizo na wateja wenye vyeti vya namba hizo.”

Zoezi la kutoa chanjo ya UVIKO-19 lilizinduliwa Julai 28, 2021 na Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo hadi kufikia Agosti 4, 2021 jumla ya dozi 1,008,400 za chanjo za UVIKO-19 zilikuwa zimesambazwa katika mikoa yote 26 na vituo zaidi ya 550 vya kutolea huduma za chanjo kwa Tanzania Bara.

Kuhusu zoezi la utoaji chanjo, Prof. Makubi amesema kuwa tangu zoezi hilo kuzinduliwa mwitikio umekuwa mkubwa miongoni mwa wananchi ambapo tayari watu 105,745 wamechanjwa hadi kufikia Agosti 7, 2021.