Naibu Waziri Gekul: Mazoezi mara tatu kwa wiki

0
278

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul ametoa rai kwa  uongozi wa wilaya ya Iringa kuhamasisha watumishi wa umma, taasisi mbalimbali pamoja na wananchi kushiriki mazoezi ili kuimarisha afya zao hatua itakayowasaidia kufanya shughuli za maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Gekul ametoa rai hiyo tarehe 7 Agosti, 2021 mjini Iringa, akiwa mgeni rasmi katika mbio za ASAS Half Marathon zilizofanyika mkoani humo.

“Mkuu wa Wilaya ya Iringa, nikuombe uandae utaratibu kwa watumishi kushiriki mazoezi angalau mara tatu kwa wiki ili waweze kuimarisha afya  zao ambazo” amesema Puline Gekul.

Naibu Waziri Gekul ameipongeza kampuni ya ASAS, kwa kuandaa mbio hizo kwa mara ya kwanza na kutoa rai mbio hizo kuendelezwa na kusisitiza umuhimu wa wadau wengine kuandaa mbio mbalimbali ili kuibua vipaji vya wanamichezo na kuimarisha afya zao.

Mbio hizo zimeshirikisha wakimbiaji kutoka katika mikoa mbalimbali nchini, wasanii pamoja na watu mashuhuri ambapo washindi wa kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake kila mmoja amezawadiwa Ng’ombe  wa Maziwa mwenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni nne pamoja na fedha taslimu kwa washindi wa pili na watatu.