Waisrael waanza kuingia nchini

0
128

Kundi la kwanza la watalii 150 kati ya 550 kutoka nchini Israel, limewasili nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro-(KIA) na kusema kuwa wameridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuhakikisha usalama wao dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19 unakuwepo muda wote.

Wakizungumza mara baada ya kutua katika uwanja huo watalii hao wamesema hatua hizo zimewaongezea hamasa ya kuona vivutio mbalimbali nchini, ikiwemo eneo la mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Serengeti.

Kiongozi wa watalii hao Shilome Carmel, amesema mara baada ya kumaliza ziara yao wana matumaini watakuwa mabalozi wazuri katika kuitangaza Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea watalii hao Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela, amesema ujio huo ni muhimu na unapaswa kuhudumiwa vyema ili wawe mabalozi wazuri kwa nchi yetu huku Mwenyekiti wa bodi ya Utalii Nchini Jaji Thomas Mihayo nae amesema hadi kufikia mwisho wa mwezi Agosti watalii zaidi ya 900 kutoka nchini Israel wanatarajiwa kutembelea vivutio mbalimbali nchini.