NARCO yaelekezwa kuipatia kitalu kampuni ya Chobo

0
191

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuipatia Kampuni ya Chobo Kitalu Mbadala katika eneo la Mradi wa Mwisa II lililopo Wilayani Muleba, Mkoani Kagera baada ya kuchelewa kuendeleza Kitalu cha awali alichopewa katika Ranchi ya Mabale na kupelekea wawekezaji wengine kutumia eneo hilo.

Ndaki ametoa agizo hilo alipokutana na mwekezaji huyo jijini Dodoma na kukubaliana kuwa Wizara itampatia eneo lingine katika mradi wa Mwisa II ili aweze kuendeleza uwekezaji katika sekta ya mifugo.

Kufuatia makubaliano hayo, Waziri Ndaki ameielekeza NARCO kushughulikia jambo hilo kwa haraka ili mwekezaji huyo aweze kuendelea na shughuli zake za uwekezaji nchini.

“Kama nilivyosema sisi tuko tayari kushirikiana na Chobo pamoja na wawekezaji wengine kwa lengo la kuongeza tija kwenye sekta ya mifugo ili kutimiza malengo ya Tanzania ya Viwanda,” amesema Ndaki

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Chobo, John Chobo pamoja na kumshukuru Waziri kwa hatua hiyo, amesema kuwa uamuzi huo utasaidia kiwanda chake kupata malighafi iliyobora kutoka kwa mifugo watakayoiwekeza katika eneo hilo na anaamini kwa ushirikiano wanaopata kutoka kwa NARCO na Wizara wataweza kuzalisha bidhaa bora itakayoweza kushindana katika Soko la Kimataifa.