Kikosi cha timu ya Simba kimerejea mkoani Dar es salaam baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya kombe la Azam Sports Federation 2020/2021, kwa kupata ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya mahasimu wao Yanga katika uwanja wa CCM Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, wachezaji wa timu hiyo wamejinasibu na kutamba kwa kufanikiwa kutetea ubingwa wao mbele ya mpinzani wao wa jadi Yanga, na kuahidi kufanya vizuri zaidi msimu ujao.
Kikosi cha Simba kimewasili mkoani Dar es salaam na kupokewa kwa mbwebwe na mashabiki wao waliojitokeza kwa wingi kuwalaki nyota wao waliofanikiwa kutetea makombe yote mawili msimu huu, Ligi Kuu Tanzania Bara na kombe la Shirikisho nchini.