Simba SC bingwa Kombe la Shirikisho

0
539
Kiungo wa Simba SC, Thadeo Lwanga (Injinia) akishangilia kwa kuvua jezi baada ya kuifungia timu yake goli katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Simba SC imetetea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuwafunga watani wa jadi, Yanga SC katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Goli pekee na la ushindi katika mchezo huo limewekwa kimyani na Thadeo Lwanga (Injinia) dakika 79. Katika michezo yote ya ASFC, Simba imefunga jumla ya magoli 14, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja.

Kwa ushindi huo, Simba inaweka rekodi ya kuwa timu iliyochukua ubingwa mara nyingi zaidi ikiwa imebeba kombe hilo mara tatu, kati ya fainali sita zilizochezwa. Yanga, Azam na Mtibwa kila moja imechukua kombe hilo mara moja.

Kumalizika kwa mchezo huo kunafunga pazia la mashindano ya kandanda kwa msimu wa mwaka 2020/2021 ambapo Simba inamaliza kibabe zaidi ikiwa na makombe matatu, ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho.

Yanga wao wamemaliza msimu wakiwa na ubingwa mmoja wa Kombe la Mapinduzi ambapo waliwafunga watani wao Simba SC kwa mikwaju ya penati 4-3 katika fainali zilizopigwa visiwani Zanzibar Januari 13, 2021.