Mashabiki wa Burundi na DRC kushuhudia mpambano wa watani wa Jadi

0
158

Mashabiki wa soka kutoka Burundi na Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC), wameanza kuwasili katika manispaa ya Kigoma – Ujiji, kwa ajili kushuhudia mpambano wa kihistoria wa watani wa jadi Simba na Yanga utakaochezwa kwa mara ya kwanza tangu kurejea kwa mashindano ya kombe la Shirikisho.

Mchezo huo utachezwa kwenye dimba la Lake Tanganyika, ambalo limefanyiwa ukarabati mkubwa tayari kwa mpambano huo.

Kuwepo kwa mpambano huo unaotarajiwa kuhudhuriwa na mashabiki elfu 60 mkoani Kigoma, kumetajwa kuwa ni sehemu ya kuufungua mkoa huo kibiashara ambapo bidhaa nyingi za mkoa huo zitaweza kufahamika.

Tiketi za kuingia katika dimba hilo.la Lake Tanganyika kwa ajili ya kuangalia mpambano.huo wa watani wa jadi zimeanza kuuzwa, na TBC imeshuhudia misururu mirefu ya mashabiki wakinunua tiket hizo.

Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema mkoa huo upo tayari kuwapokea mashabiki kutoka pande zote, na kuna miundombinu ya kutosha kuwawezesha mashabiki hao kupata huduma wanazotaka.

Amesema ulinzi umeimarishwa katika kipindi chote cha kabla na baada ya mpambano huo mkubwa.

Akizungumzia juhudi za Serikali katika kuboresha usafiri wa majini, Andengenye amesema kwa sasa Serikali ina mpango wa kukarabati meli mbili za MT Sangara na MV Lihemba, ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji pamoja na kukuza shughuli za kiuchumi.

“Rais wetu Samia Suluhu Hassan alisaini mkataba wa kukarabati meli mbili na ujenzi wa meli mbili zingine mpya zitakazotumika katika ziwa Tanganyika.” Amesema Andengenye