Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, -Simba wanashuka dimbani jioni ya leo katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuumana na timu ya KMC ya Kinondoni katika mchezo wa kiporo kwenye mfululizo wa ligi hiyo.
Simba yenye alama 27 baada ya kushuka dimbani mara 12, ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo ambapo itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya KMC iliyo katika nafasi ya tisa ikiwa imejikusanyia alama 21.
Mabingwa hao watetezi wako nyuma kwa alama 17 dhidi ya vinara wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, -Yanga wenye alama 44 baada ya kucheza michezo 16 huku wakifuatiwa na Azam walio kwenye nafasi ya pili baada ya kujikusanyia alama 40 katika michezo 16.
Ligi hiyo itaendelea Alhamisi Disemba 20 mwaka huu, kwa mchezo mmoja kupigwa huko mkoani Arusha ambapo African Lyon waliohamishia michezo yao ya nyumbani kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid wanawaalika vinara wa ligi hiyo, timu ya Yanga.