Man U yapata kocha wa muda

0
1356

Klabu ya Manchester United ya nchini England  imemtangaza mchezaji wake wa zamani, –  Ole Gunnar Solskjaer kama kocha wake wa muda mpaka mwisho wa msimu huu,  kuchukua mikoba ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mreno Jose Mourinho aliyefukuzwa kazi.

Kocha huyo aliyeichezea Manchester United michezo 235 na kuifungia mabao 91, anachukua majukumu ya kukiongoza kikosi hicho kikiwa katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi kuu ya England.

Akiongelea kupewa majukumu hayo, -Solskjaer amesema kuwa  amefurahishwa sana na kurudi tena klabuni hapo kwa sababu klabu hiyo bado ipo moyoni mwake huku Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa klabu hiyo, -Ed Woodward akisema kuwa Solskjaer ana vinasaba na Man United ndio maana wamempa jukumu hilo.

Kutangazwa kwa Solskjaer mwenye miaka 45 raia wa Norway kurithi mikoba ya Mourinho,  kunahitimisha uvumi ulioenea kufuatia tangazo lililotolewa kimakosa na Manchester United likimtambulisha kocha huyo anayekinoa kikosi cha Molde cha nchini Norway hivi sasa.

Tangazo hilo lililowekwa kwenye tovuti ya klabu hiyo likisindikizwa na bao la nyota huyo alilofunga kwenye fainali ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya mwaka 1999 akiichezea Manchester United, lilifutwa muda mchache baadaye,  hali iliyoibua mijadala.

Tangazo hilo lilisababisha Waziri Mkuu wa Norway, -Erna Solberg kutumia ukurasa wake wa  mtandao wa kijamii wa Twitter kumtakia kila la kheri kocha huyo katika safari ya kukinoa kikosi hicho huku akisema kuwa ni siku kubwa sana kwa soka la Norway kwa Solkjaer kupata nafasi ya kuwa kocha mkuu wa muda wa Manchester United.

Hata hivyo, muda mchache baada ya Manchester United kufuta taarifa ya kumtambulisha Solkjaer, Waziri Mkuu wa Norway naye akauondoa ujumbe wake wa kumtakia kila la kheri Sosha.

Ole Gunnar Solkjaer aliichezea Manchester United kuanzia mwaka 1996 mpaka mwaka 2007 huku akipata nafasi ya kufundisha timu ya akiba ya Manchester United kwa miaka mitatu tangu alipostaafu kucheza soka mwaka 2007 hadi mwaka 2010.

Solkjaer atasaidiwa na aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo enzi za Sir Alex Ferguson huku Michael Carrick na Kieran McKenna waliokuwa wasaidizi wa Mourinho nao wakiendelea kuwa chini ya Ole Gunnar Solskjaer.