Tarimba: Ukurasa wa Twitter upuuzwe, sio hoja zangu

0
178

Mbunge wa jimbo la Kinondoni mkoani Dar es Salaam kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abbas Tarimba amesema hausiki na ukurasa uliopo kwenye mtandao wa Twitter unaosomeka kwa jina lake.

Katika mahojiano na TBC mkoani Dar es Salaam, Tarimba amesisitiza kuwa hoja zilizoandikwa katika ukurasa huo si zake, na wala yeye si muhusika wa ukurasa huo.

“Sikuwahi kufikiria agenda kama hizo na sio hoja zangu, suala hili limepenyezwa kwa lengo la kunivunjia heshima.” amesema Tarimba.

Katika ukurasa huo wa Twitter wenye jina la Tarimba Abbas imeandikwa “Bunge lijalo nimedhamiria kupeleka muswada wa sheria wa mabadiliko ya stahiki za posho za Wabunge kukatwa kodi na kuchangia katika mifuko ya jamii.” Jambo ambalo Tarimba amekanusha kuhusika nalo.