Serikali : Watanzania Afrika Kusini wapo salama

0
262

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema mpaka sasa hakuna taarifa za Mtanzania yeyote aliyedhurika ama kukamatwa kwa kujihusisha na vurugu na maandamano yanayoendelea katika baadhi ya miji nchini Afrika Kusini, kushinikiza kuachiwa kwa Rais Mstaafu wa nchi hiyo Jacob Zuma.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na wizara hiyo imeeleza kuwa Serikali kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini unaendelea kufuatilia na kuwasiliana na Viongozi wa Jumuiya za Watanzania wanaoishi nchini humo, Mamlaka na vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kufahamu endapo kuna Mtanzania yeyote aliyehusishwa ama kudhurika katika tukio hilo.

“Kama Serikali ya Afrika Kusini inavyoelekeza, Ubalozi wa Tanzania Afrika Kusini unawasihi Watanzania waliopo hapa kuendelea kuwa watulivu na kutojihusisha na vurugu pamoja na maandamano yanayoendelea nchini hapa.” amesema Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi
 
Balozi Milanzi ameongeza kuwa, kwa sasa Serikali ya Afrika Kusini imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha vurugu hizo zinadhibitiwa, ili zisisambae katika maeneo mengine na kwamba Jeshi la Ulinzi la Afrika Kusini limeelekezwa kuungana na jeshi la polisi katika kudhibiti vurugu hizo.
 
Maandamano na vurugu nchini Afrika Kusini zilianza wiki iliyopita, kupinga hukumu iliyotolewa dhidi ya Rais Mstaafu wa nchi hiyo Jacob Zuma ya kutumikia kifungo cha miezi 15 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuidharau mahakama.