Rais Samia : Mzee Mkapa alikuwa gwiji wa mageuzi ya kiuchumi

0
148

Rais Samia Suluhu Hassan, amesema aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania Hayati Mzee Benjamin Mkapa alikuwa gwiji wa mageuzi nchini, ambapo aliweza kusimamia ukusanyaji wa kodi na ulipaji wa madeni ya Taifa.

Akihutubia Kongamano la Kumbukizi ya mwaka mmoja tangu kifo cha Mzee Mkapa, Rais Samia Suluhu Hassan amesema wakati wa uongozi wake kiongozi huyo alisimamia ukusanyaji wa kodi na kuanzisha taasisi nyingine ambazo mpaka leo zinaendelea kuwahudumia Wananchi.

Rais Samia amesema, Hayati Mkapa alianzisha taasisi kama Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) , Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), MKUKUTA na MKURABITA pamoja na taasisi nyingine nyingi zilizolenga kuwainua Wananchi kiuchumi.

Amesema Hayati Mzee Mkapa pia alisimamia uanzishwaji wa mpango wa maendeleo ya Taifa wa mwaka 2020-2025 ambao umeonesha mafanikio makubwa kwa Taifa.

Rais Samia Suluhu Hassan pia amemuelezea Hayati Mzee Mkapa kama Kiongozi aliyefanikiwa sana kupunguza deni la Taifa, ambapo wakati anaingia madarakani Tanzania ilikuwa inadaiwa madeni yanayofikia asilimia 143.7 na mwaka 2005 alipunguza deni hilo na kufikia asilimia 60.7.

Amemuelezea Mzee Mkapa kama Kiongozi aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kushawishi Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwashawishi wahisani kuisamehe Tanzania madeni yake na kuifanya kuweza kukopesheka tena.

Kuhusu Utandawazi, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Mzee Mkapa alikuwa Kiongozi aliyeamini katika Utandawazi na kwamba yeye pamoja na Rais wa zamani wa Finland Tarja Halonen waliongoza Tume ya Utandawazi Duniani.