Kikwete: Hayati Mkapa amefanya mambo makubwa

0
145

Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete amesema aliyekuwa mtangulizi wake, Hayati Benjamin Mkapa amelifanyia Taifa la Tanzania mambo makubwa, na ndio maana mpaka sasa anakumbukwa.

Akizungumzia maisha ya Hayati Mkapa katika Kongamano la Kumbukizi ya mwaka mmoja tangu alipofariki dunia, Dkt. Kikwete amesema Mzee Mkapa alianzisha taasisi nyingi ikiwa ni mkakati wake wa kuifikisha nchi katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Rais Mstaafu Kikwete ameongeza kuwa katika sekta elimu Hayati Mkapa alianzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES), mipango iliyolenga kuboresha kiwango cha elimu katika ngazi hizo.

Ameongeza kuwa katika uongozi wake Hayati Mkapa alianzisha Taasisi zilizotoa huduma kwa haraka kwa Wananchi ambazo pia zililenga kutekeleza malengo ya Milenia na pia mpango wa Taifa wa maendeleo.

Kwa upande wa Afya, Hayati Mzee Mkapa alianzisha Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) ikiwa ni jitihada za Serikali za kukabiliana na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ya Ukimwi lakini pia alianzisha programu mbalimbali za kuboresha afya kwa Watanzania.