Chongolo: Ujenzi wa Barabara ya Igawa-Tunduma kuanza mara moja

0
184

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amewahakikishia wakazi wa mkoa wa Mbeya kuwa ujenzi wa barabara kuu kutoka Ugawa – Mbeya hadi Tunduma yenye urefu wa zaidi ya kilomita 200 utaanza mara moja, na kuuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha inakamilisha michoro ya upembuzi haraka iwezekanavyo.

Chongolo ametoa ahadi hiyo jijini Mbeya wakati akizungumza na Wakazi wa eneo la Uyole, aliposimama kuwasalimia Wakazi hao akielekea katika ziara yake ya kutembelea mashina ya CCM eneo la Nsalaga.

Chongolo amewataka wakazi hao wa jiji la Mbeya kuendelea kuiamini CCM, na kwamba ujenzi wa barabara hiyo ya njia nne utafanyika ili kupunguza foleni ya magari iliyopo sasa.

Pia amekagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya Chief Rockert Mwashinga, mali ya halmshauri ya jiji la Mbeya, na kueleza kuridhishwa na ujenzi huo.

Katibu Mkuu huyo wa CCM ametembelea na kukagua ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, ambalo litagharimu zaidi ya shilingi bilioni nane hadi kukamilika kwake na kwa sasa ujenzi huo umefikia asilimia 85.