Wakazi wa kijiji cha Maweni kata ya Mkwajuni wilayani Songwe, wameamua kujitolea nguvu zao kushiriki ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya msingi Maweni.
Wakizungumza na mwandishi TBC mkoani Songwe, Wakazi hao wamesema wameamua kushiriki ujenzi huo, ili kuihamasisha jamii kuchangia nguvu zao kushiriki shughuli za maendeleo.
Wamesema hamasa ya kushiriki shughuli hiyo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa wameipata kutoka kwa Viongozi wao ambao waliwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kushiriki kwenye shughuli za maendeleo.
“Kushiriki katika shughuli za maendeleo ni muhimu kwa sababu kwanza inawapa fursa ya kuwa na uchungu na miradi, mwanzo tulikuwa na elimu duni juu ya kushiriki kwenye shughuli hizo lakini baada ya diwani na uongozi kutoka elimu Wananchi tumekua na mwamko mkubwa sana.” amesema Mawazao Mwakagile, mkazi wa kijiji cha Maweni.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mkwajuni, Shaibath Kapingu amesema kwa sasa wanajenga vyumba hivyo vitatu vya madarasa, lakini wataendelea kujenga vyumba zaidi kwa kuwashirikisha Wananchi.