Kilo 1.2 ya heroin yawafikisha mahakamani

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

0
158

Watu watatu wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mkoani Dar es salaam, wakikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin kilo 1 na gramu 200.

Washtakiwa hao ni Andrew Paul, Said Mugoha na Geroge Mwang’ata wote wakazi wa Temeke mkoani Dar es salaam.

Akiwasomea washtakiwa hao shtaka lao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Ritha Tarimo, Wakili wa Serikali Yusuf Aboud amedai washtakiwa hao wametenda kosa hilo Juni 21 mwaka huu maeneo ya Mivinjeni katika manispaa ya wilaya ya Temeke.

Mara baada ya washtakiwa hao kusomewa shtaka lao hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa mujibu wa sheria.

Aidha wakili Aboud amedai upepelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo kuomba Mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 27 mwezi huu kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote wamerudishwa rumande.