Ndaki amaliza mgogoro wa Ardhi ranchi ya Kagoma

0
143

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameumaliza mgogoro wa ardhi kati ya wananchi waliovamia kwenye vitalu katika Ranchi ya Kagoma na wawekezaji ambao wanamiliki vitalu hivyo.

Waziri Ndaki ameumaliza mgogoro huo baada ya kuwasikiliza wananchi na wawekezaji kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Rutoro wilayani Muleba Mkoa wa Kagera.

Akizungumzia kuhusu mgogoro huo, Waziri Ndaki amewaeleza wananchi kuwa maeneo hayo waliyoyavamia ni mali ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambayo tayari yalikuwa yameshakodishwa kwa wawekezaji wanaofanya shughuli za ufugaji hivyo walipaswa kuondolewa. Lakini kutokana na busara za Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia eneo hilo lipimwe na wananchi wabakizwe kwenye vijiji vinne vilivyopo ambavyo ni Kijiji cha Rutoro, Byengeregere, Chobuheke na Mishambya vilivyopo katika Kata ya Rutoro.

Aidha amewataka wananchi kutoendelea kuvamia maeneo mengine katika ranchi hiyo kwani wakifanya hivyo kwa sasa watachukuliwa hatua.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila amemuhakikishia waziri kuwa maelekezo aliyoyatoa watakwenda kuyasimamia kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Kagera na uongozi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).

Kutokana na uamuzi uliochukuliwa wa kupima maeneo hayo kwenye ranchi ya Kagoma, wawekezaji na wananchi wote wameonesha mtazamo chanya kwani hata wao wenyewe hilo ndio wameliona ndio suluhisho.