Tanzania ina wagonjwa 408 wa corona

0
185

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema hadi kufikia tarehe 8 mwezi huu, Tanzania imerekodi wagonjwa 408 wa corona, tangu wimbi la tatu la ugonjwa huo lilipoingia nchini.

Waziri wa wizara hiyo Dkt. Dorothy Gwajima amesema kati ya wagonjwa hao,  284 wanapumua kwa usaidizi wa mashine za oksijeni katika hospitali mbalimbali nchini.

Dkt. Gwajima ametoa takwimu hizo mkoani Dodoma katika mnada wa Msalato, ilipokuwa inatolewa elimu ya namna ya kujikinga na corona.

Kufuatia kuwepo kwa wimbi hilo la tatu la corona nchini, Dkt. Gwajima amewaagiza viongozi wa mikoa na wilaya nchini kutumia njia mbalimbali kufikisha elimu kwa Wananchi ya namna ya kujikinga na corona, ikiwa ni pamoja na kutumia redio za kijamii.

Waziri huyo wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pia amefanya ziara katika  hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma, kuona namna ilivyojipanga katika kuwahudumia wagonjwa wa corona.