Wawekezaji NARCO watakiwa kufuata taratibu za mikataba

0
183

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wawekezaji kwenye vitalu vya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kufuata taratibu zilizowekwa kulingana na mikataba yao.

Ndaki ameyasema hayo wilayani Misenyi mkoa wa Kagera wakati alipotembelea Ranchi ya Mabale na kuzungumza na baadhi ya wawekezaji wenye mifugo katika vitalu hivyo na kueleza kuwa ipo tabia ya baadhi ya wawekezaji kuchukua vitalu na kutovitumia kama ilivyoelekezwa kwenye mikataba kitu ambacho kinasababisha maeneo kuwa mapori na kuvamiwa na watumiaji wengine wa ardhi.

Wizara kupitia NARCO imejipanga kuhakikisha wafugaji wanapata maeneo ya vitalu kwa ajili ya kufugia kitu ambacho kitasaidia kuondokana na tatizo la malisho na kupunguza migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine.

Vilevile amesema wizara kwa sasa inaiona NARCO kama ni sehemu ya kutokea kwani kupitia kampuni hiyo wizara itaweza kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuongeza kipato wa wafugaji.

Akiwa katika Ranchi hiyo Waziri Ndaki amemtaka mwekezaji wa Kampuni ya Chobo Investment kuachia eneo analolimiliki kwa sasa wakati akiendelea kujipanga ili wawekezaji wengine ambao tayari wanayo mifugo waweze kulitumia.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara imejipanga kuhakisha uzalishaji wa Mifugo na mazao yake unaongezeka na kuhakikisha wawekezaji katika sekta wanasaidiwa ili wasikwame katika uwekezaji wao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wawezekaji hao wamemweleza waziri kuwa bado wanahitaji maeneo kwa ajili ya kufugia na kuwa wanaishukuru serikali kupitia NARCO kwa ajili ya kutenga maeneo hayo na kuwashushi gharama ya ukodishaji wa vitalu.