Mchezaji wa Polisi Tanzania avunjika miguu ajalini

0
316

Na Sauda Shimbo, Moshi

Wachezaji 16, kocha msaidizi na dereva wa timu ya Polisi Tanzania wamelazwa katika Hospitali ya KCMC baada ya kupata ajari hii leo huko mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Ajali hiyo imetokea kwenye eneo la Mkababuni barabara ya TPC, Moshi wakati wachezaji hao wakirejea kutoka mazoezini.

Akizungumza mara baada ya kuwatembelea na kuwajulia hali zao, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema chanzo cha ajali hiyo ni gari kuacha njia na kugonga mti upande wa kushoto mwa barabara na kusababisha majeruhi hao.

Gari hiyo yenye namba PT. 4043 Ashok Layland ni basi la Shule ya Polisi Moshi ambapo wachezaji hao walikuwa wakielekea shuleni hapo.

Nahodha wa timu hiyo, Mohammed Othman anasema hawakuona chochote wakati ajali hiyo inatokea, lakini amewatoa hofu Watanzania kwamba wanaendelea vizuri na matibabu.

Katika ajali hiyo mchezaji Gerald Mdamu ndio ameumia zaidi baada ya kuvunjika miguu yote miwili.