Klabu ya Manchester United ya nchini England imetangaza kumfuta kazi meneja wake Jose Mourinho.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imemshukuru Mourinho kwa kazi aliyoifanya muda wote aliokua akifanya kazi na klabu hiyo na imemtakia kila la kheri kwa siku zijazo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa meneja wa muda atakayeiongoza klabu hiyo hadi mwishoni wa msimu, atatangazwa wakati wowote kuanzia sasa wakati uongozi wa klabuĀ hiyo ya Manchester United ukitafuta meneja wa kudumu.
Mourinho, Raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 55 amefukuzwa kazi baada ya kuingoza klabu hiyo kwa muda wa miaka miwili na nusu, huku akiipatia timu hiyo taji la Europa na kombe la ligi.
Manchester United imekubali kipigo cha mabao matatu kwa moja kutoka kwa Liverpool mwishoni mwa juma, kipigo kinachoiweka timu hiyo nyuma kwa alama 19 dhidi ya vinara hao wa Ligi Kuu ya England.
Mourinho anaondoka klabuni hapo wakati ambapo droo ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya ikiwa imetangazwa na Manchester United imepangwa kucheza na PSG ya Ufaransa.