Ulinzi Mgodi Wa Tanzanite Wazidi Kuimarishwa

0
150

Serikali imeamua kuimarisha ulinzi eneo la mgodi wa Tanzanite Mirerani mkoani Manyara, ili kulinda madini hayo ambayo yanapatikana nchini Tanzania pekee.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, baada ya kuzindua kituo cha madini cha ‘Magufuli One Stop Center’ ambacho kitasaidia ukataji na upandishaji thamani wa madini ya Tanzanite kabla ya kuingia sokoni.

“Tanzanite hii ndiyo inayotusaidia kupata fedha za maeneo mengine hivyo lazima serikali inagalie kwa jicho la pekee ili kuhakikisha wananchi wa eneo hili wanatimiza malengo yao kupitia eneo hili,”amesema Majaliwa.

Pia amebainisha kuwa kulindwa kwa rasilimali hiyo itasadia kuepusha utoroshwaji wa madini ya Tanzanite kwenda kuuzwa kwenye nchi zingine kiholela.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka ameiomba Serikali kuhakikisha inajenga soko la madini Mirerani ili kurahisisha uuzaji wa madini hayo.

“Madini yanayozalishwa hapa yamekuwa yakisafirishwa kwenda kuuzwa kwenye miji mikubwa na nchi jirani hivyo Serikali ikitatua hiyo changamoto ya soko maisha ya wanchi yanakotoka madini yatainuka kuwa juu zaidi,”amesema Ole Sendeka.

Mbunge huyo pia ameiomba serikali kuwepo na ukaguzi wa staha kwa wachimbaji na wananchi wanaoingia na kutoka kwa ajili kutoa huduma eneo la mgodi huo.