Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken.
Wakati wa mazungumzo hayo Waziri Blinken amemuhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuleta maendeleo kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) kwa kuzingatia vipaumbele vya nchi.
Amempongeza kwa hatua anazozichukua katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona, na kuongeza kuwa Marekani ipo tayari kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Pia amepongeza jitihada za Rais katika kuimarisha demokrasia nchini, ikiwa ni pamoja na azma yake ya kukutana na kushirikiana na vyama vya siasa, pamoja na kusimamia uhuru wa vyombo vya habari.
Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi Serikali yake kuendelea kushirikiana na Marekani kukuza uhusiano baina ya nchi hizo mbili katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa.
Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mwaliko kwa Rais wa Marekani Joe Biden kutembelea Tanzania ili kuzidi kuimarisha uhusino uliopo kati ya nchi hizo mbili.