serikali yaagiza kufanyika tafiti uwepo wa migongano ya wanyama na binadamu

0
157

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro ameuagiza uongozi wa Chuo Usimamizi wa Wanyapori – Mweka kilichopo mkoani Kilimanjaro kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), kufanya utafiti wa kujua sababu za kuongezeka kwa migongano na migogoro kati ya wanyama wakali waharibifu na binadamu.

Akizungumza na watumishi wa chuo hicho, Waziri Ndumbaro amesema siku zote katika utafiti usiamini jibu ulilonalo hadi pale unapofanyia jambo hilo utafiti ili kujua ukweli zaidi.

“Tunaomba tafiti nyingi sana zielekezwe huko ili mje na majibu kwanini vurugu hizi zinaendelea kuongezeka badala ya kupungua.”ameagiza Waziri huyo wa Maliasili na Utalii

Amesema ikiishajulikana sababu utapatikana ufumbuzi wa tatizo hilo, na hivyo kuondoa kadhia ambayo jamii imekua ikiipata.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho cha Usimamizi wa Wanyamapori – Mweka Profesa Japhary Kideghesho amesema kuwa, wamekuwa wakifanya tafiti katika maeneo ya muingiliano wa binadamu na wanyamapori, lakini kwa agizo hilo la Dkt. Ndumbaro watajielekeza kufanya tafiti maeneo yaliyoathirika zaidi na tatizo hilo.