Dkt. Mpango : Biashara ni ushindani

0
226

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewashauri Wafanyabiashara nchini kuboresha biashara zao, ili ziweze kushindanishwa katika soko la dunia.

Dkt. Mpango ameyasema hayo wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Dar es salaam, maarufu kama Sabasaba.

“Ni muhimu sana kwa wazalishaji wetu wa ndani kukumbuka siku zote biashara ni ushindani, kuna ushindani mkali wa biashara.” amesisitiza Dkt. Mpango.

Pia amewasisitiza Wafanyabiashara nchini kuzingatia mahitaji ya soko na masharti ya mikataba walioingia na wateja wao, ikiwa ni pamoja na kuzingatia viwango vya bidhaa, bei na muda wa kufikisha huduma sokoni.

Makamu wa Rais amesema ujanja ujanja au kukosa uaminifu kunaua biashara, na kunasababisha kupoteza masoko ya uhakika.

Ameishauri Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), kuandika kitabu kuhusu maonesho ya Sabasaba, kuzingatia malengo mahususi ya maonesho hayo ya Sabasaba pamoja na kuwepo na vigezo vya kupima kiwango cha mafanikio yake.