Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Profesa Godius Kahyarara amesema Serikali inaendelea na mkakati wa kuanzisha vituo vya biashara vya kimataifa katika maeneo ya mipakani, ili kuwezesha ununuzi wa bidhaa za Tanzania kwa urahisi.
Profesa Kahyarara ametoa kauli hiyo jijini Dodoma, wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa maofisa biashara kutoka mikoa yote nchini.
“Watu wanapokuja kununua bidhaa za Kitanzania sio lazima waendeshe gari kutoka Namanga mpaka Tunduma, hii ni fursa kama tukiambiwa kuna ardhi tutawaita wawekezaji wataenda kuangalia maeneo hayo,
tutahakikisha wanaweka vitendea kazi kwa ajili ya kupima ubora wa mazao kama ni mahindi na vitu vingine basi vipimwe hapo hapo mpakani.”Amesema Profesa Kahyarara.
Pia amesisitiza maofisa biashara kote nchini kuandaa kanzi data ya ardhi, ambayo itaonesha maeneo ya uwekezaji katika mkoa husika.
Kwa upande wake Meneja wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kanda ya Kaskazini Daudi Riganda amesema kuwa, lengo la mafunzo hayo kwa maofisa biashara nchini ni kuwafundisha namna ya kuwahudumia Wawekezaji katika maeneo yao.