Joto kali laitesa Canada na Marekani

0
188

Zaidi ya watu mia moja wamefariki dunia kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha joto katika maeneo kadhaa nchini Canada pamoja na Marekani.

Mamlaka za hali ya hewa katika nchi hizo zimeeleza kuwa, ongezeko hilo la joto limefikia nyuzi 45 na katika baadhi ya maeneo limefika hadi nyuzi joto 50.

Wataalamu wa afya katika maeneo mbalimbali ya nchi hizo za Canada na Marekani wamesema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka kutokana na kuendelea kuwepo kwa joto kali.

Hali inaelezwa kuwa mbaya zaidi katika majimbo ya Oregon nchini Marekani pamoja na Vancouver na British Columbia ya nchini Canada.

Ongezeko hilo la kiwango cha joto limetokana na mgandamizo wa hewa kutoka maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa nchi hizo, huku kiini chake kikitajwa kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamechochewa na shughuli za kibinadamu.

Waziri Mkuu wa Canada,  Justin Trudeau ametuma salamu za pole kufuatia vifo vilivyotokea nchini mwake, ambapo wengi wa waliofanriki dunia ni watu wenye umri mkubwa.