Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefungua mafunzo ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa, na kuwataka waendelee kusimamia amani na utulivu kwenye mikoa yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote.
Mafunzo hayo ya siku nne yanayofanyika jijini Dodoma, yameandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa lengo la kuwaimarisha viongozi hao.
“Amani na utulivu ndiyo itatuwezesha kama nchi tuendelee kuwavutia Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza mitaji yao hapa nchini, tunakumbushwa sisi viongozi tuwe wazalendo na tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali za nchi hii kwa faida ya Watanzania wote.” Amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema baada ya mafunzo hayo Serikali inatarajia kuona Viongozi hao wanasimamia kikamilifu nidhamu katika utumishi wa umma na kuwa kioo katika kuzingatia maadili na miiko bila kubagua jinsia, kabila, dini ama rangi ya mtu.