Waziri Mkuu : Chukueni tahadhari ya corona

0
146

Serikali imeendelea kuwasisitiza Wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona, ambao tayari wimbi la tatu la ugonjwa huo limeingia katika baadhi ya maeneo nchini

Kauli hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiahirisha Bunge la 12.

Amesema ni muhimu kwa Wananchi wa maeneo mbalimbali wakachukua tahadhari wawapo kwenye maeneo yao ya kazi, usafiri wa umma na kwenye nyumba za ibada.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema tahadhari za awali ambazo zinaweza kuchukuliwa ni pamoja na kuvaa  barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka ama kwa kutumia vitakasa mikono na kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu hasa katika maeneo yenye misongamano.

Amesema kwa upande wa Serikali, tayari imeanza kuchukua hatua katika kukabiliana na ugonjwa wa corona ikiwa ni pamoja na kusitisha safari za ndege kutoka na kwenda kwenye nchi zilizoathirika zaidi na corona, kuimarisha ukaguzi kwa wasafiri na kuimarisha kazi ya upimaji virusi vya corona.