Wananchi laki 3.5 wanufaika na Taasisi ya Mkapa

0
162

Serikali mkoani Kilimanjaro imesema uwepo wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation mkoani humo, imewasaidia wananchi wengi kupata huduma za afya kwa wakati hasa akina mama wajawazito na watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili katika maeneo ya vijijini.

Akizungumza wakati wa kutathmini shughuli za taasisi hiyo mkoani Kilimanjaro katika kuelekea kumbukumbuku ya Mwaka mmoja tangu kifo cha Hayati Rais Benjamin Mkapa, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Jonas Mcharo amesema tangu taasisi hiyo ilipoanza kutoa huduma zake mkoani humo mwaka jana tayari imetoa wahudumu wa ngazi ya jamii 279.

Mcharo amesema wananchi wapatao laki 3.5 wamenufaika na huduma za afya kupitia Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation katika Halmashauri tatu, ikiwemo Halmashauri ya wilaya ya Moshi, Manispaa ya Moshi na wilaya ya HAI.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Hai George Massawe, amesema tayari Taasisi hiyo imetoa huduma katika kata zote 17 kupitia wahudumu 62 katika vijiji 79 wilayani Hai katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwapatia matibabu.

Mmoja wa wanufaika wa Taasisi hiyo kutoka wilayani Hai Diana Athanas amesema hapo awali hakuona umuhimu wa kuwahi kliniki akiwa mjamzito lakini BMF imempa elimu na kupata mwamko wa kuwahi kliniki.

Sauda Shimbo, Kilimanjaro.