Miradi 93 imesajiliwa siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan

0
302

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imesajili miradi 93 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.6 ambayo itaingiza ajira zaidi ya 24,600 kwa vijana.

Amesema kuwa hatua hiyo inatoa alama kwa wawekezaji wa nje kwamba kwa sasa urasimu katika sekta ya uwekezaji unaendelea kupunguzwa katika maeneo ya usajili wa makampuni pindi muwekezaji anapokusudia kuja kuwekeza nchini.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Juni 27,2021wakati akifungua kongamano la siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan lililofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere-(JNICC), jijini Dar es Salaam.

Amesema mbali na miradi hiyo, pia Rais Samia Suluhu Hassan amefanya jitihada kubwa ya kuondoa tozo 232 zilizokuwa zinawakwaza wafanyabishara.

Waziri Mkuu amesema katika kufanya kazi zake, Rais Samia Suluhu Hassan ameendeleza mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi jirani ambapo ametembelea nchi za Kenya, Uganda na Msumbiji kwa lengo la kuimarisha urafiki na Mataifa ya jirani. Pia amepokea ujumbe kutoka nchi mbalimbali ikiwa ni alama ya mshikamano.

Amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kupanga mipango ya ujenzi wa miradi mipya katika siku 100 za uongozi wake ikiwemo kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa reli ya kimataifa kipande cha kutoka Mwanza mpaka Isaka, ujenzi wa meli mpya nne na ukarabati wa meli kongwe moja.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia ameanzisha mradi wa shule za sekondari za wasichana katika halmashauri zote nchini. Pia amesema Rais ametoa shilingi milioni 500 kwa kila jimbo kwa ajili ya kukarabati barabara ili kuboresha huduma za usafiri vijijini.