Mazungumzo ya Rais na makundi yawakosha wengi

0
199

Utaratibu wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kukutana na makundi maalumu yakiwemo wazee, wanawake, vijana na viongozi wa dini nchini umepongezwa na Watanzania ambao wamesema ni njia nzuri katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu katika makundi hayo.

Pongezi hizo zimetolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Mt. Augustino, Padri Dkt. Inocent Sanga wakati wa Kongamano la Siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan madarakani lililoandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania katika chuo hicho jijini Mwanza.

Dkt. Sanga amesema kupitia makundi hayo Rais Samia Suluhu Hassan ametoa hotuba zenye kuonesha dira ya Serikali yake ikiwemo kutatua kero zinazowakabili watu wa makundi hayo.

“Katika siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya vizuri sana kwa kuamua kukutana na makundi maalumu yakiwemo wazee, wanawake, vijana, na viongozi wa dini. Kwa namna alivyofanya uteuzi kwa kuzingatia sekta mbalimbali na makundi mbalimbali,” Padri Dkt. Sanga

Kwa upande wake Dkt. Isaac Safari amesema katika siku 100 za uongozi wa Rais amejionea mengi ikiwa ni pamoja na kutoa dira nzuri katika sekta ya uwekezaji ambao utasaidia kukuza uchumi kwa Taifa.

“Rais ameonesha dira nzuri hasa katika kujali sekta binafsi na uhamasishaji wa ulipaji wa kodi kwa hiari kwa wafanyabiashara wetu. Rais ameonesha kusimamia vyema sekta ya uwekezaji, ambayo itasaidia kukuza uchumi wa Taifa maana hii ni sekta muhimu kwa nchi yeyote,” amesisitiza Dkt. Safari