Serikali yafufua mradi wa Bandari ya Bagamoyo

0
245

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeamua kufufua mazungumzo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na mradi wa Mchuchuma na Liganga ili kuchochea kasi ya kukuza uchumi nchini.

Amesema ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ni muhimu kwa sababu utaongeza uwezo wa kushindana na bandari shindani na kukuza uchumi wa Taifa.

Kuhusu mikakati ya kuzisaidia sekta za utalii na usafiri wa anga ambazo zimeathiriwa na ugonjwa wa corona, Rais Samia amesema Serikali imepunguza ada mbalimbali ikiwa ni pamoja na ada ya Wakala wa Wasafirisha Watalii kutoka Dola za Marekani 2,000 hadi Dola 500 kwa kampuni yenye magari kati ya 1 na 3.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sekta binafisi nchini (TPSF), Angelina Ngalula ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujenga mazingira bora na rafiki kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa ikiwa ni pamoja na kufuta baadhi ya kodi na tozo ambazo zimesaidia kuimarisha biashara na uwekezaji nchini.

Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) limeanzishwa likiwa ni jukwaa rasmi la majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kuwezesha kupatikana kwa muafaka wa pamoja kuhusu masuala muhimu yanayohusu maboresho ya Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu za biashara na uwekezaji nchini.