Sauda Shimbo, Rombo
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kagaigai amezitaka halmashauri za mkoa huo kuhakikisha zinatoa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya vijana, wanawake na wenye ulemavu kwa wakati ili kuinua kipato na kuziletea halmashauri maendeleo.
Agizo hilo la RC Kagaigai linafuatia uwepo wa hoja ya halmashauri ya wilaya ya Rombo ya kupeleka pungufu ya asilimia 10 ya mapato ya ndani katika mfuko wa vijana, wanawake na wenye ulemavu katika kipindi cha mwaka 2019/2020.
Kagaigai amesema kitendo cha halmashauri kutokupeleka asilimia 10 ya mapato ya ndani katika mfuko huo ni ukiukwaji wa sheria jambo ambalo serikali ya mkoa haitavumilia kuona jambo hilo likiendelea.
Amesema zipo taarifa za vijana wengi wilayani Rombo kujihusisha na vitendo vya unywaji wa pombe badala ya kufanyakazi za maendeleo, hivyo halmashauri ihakikishe inatoa fedha hizo kwa vijana ili wajikwamue kimaisha na kujipatia kipato.
Kwa upande wao baadhi ya madiwani wamesema kutokutolewa kwa asilimia 10 kwa makundi hayo kunakwamisha jitihada za serikali za kuwanyanyua wananchi kiuchumi.
Kanuni namba 5.5 [1] ya sera ya mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2019 inataka kila halmashauri kuchangia asilimia 10 ya mapato ya ndani.