Wizi wa milioni 700 wawafikisha mahakamani

0
136

Wafanyakazi watatu wa kampuni ya Tanzania Letshego Limited maarufu kwa jina la Faidika wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu mkoani Dar es salaam, wakikabiliwa na shtaka la wizi wa shilingi milioni mia saba mali ya kampuni hiyo.

Washtakiwa hao ambao ni Elisha Tengeni, Donald Kwayu na Elisha Mboka wamepandishwa kizimbani katika mahakama hiyo na kusomewa shtaka lao na Wakili wa Serikali Ester Martin akisaidiwa na Faraji Nguka mbele ya Hakimu Mkazi mkuu wa mahakama hiyo Evodia Kyaruzi.

Awali akisoma hati ya shtaka hilo Wakili Nguka amedai washtakiwa hao wakiwa Watumishi wa kampuni ya Faidika Limited walitumia nafasi zao za kazi na kujipatia fedha shilingi milioni 700 mali ya kampuni hiyo, kosa ambalo wanadaiwa kulitenda kati ya mwezi Januari mwaka 2016 na Septemba mwaka 2017.

Washtakiwa wote wamekana kuhusika na wizi huo na mahakama imeweka wazi masharti ya dhamana kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya shilingi milioni 50 kila mmoja wakati huo washtakiwa wao wakitakiwa kuwasilisha mahakamani hapo fedha taslimu shilingi milioni 350 au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Hata hivyo Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, na kuomba kupanga tarahe nyingine kutajwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 30 mwezi huu kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote wamepelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.