Tanzania kupeleka bidhaa zaidi China

0
227

China imeahidi kufungua zaidi soko lake kwa bidhaa za Tanzania, pamoja na kuongeza uwekezaji hasa katika sekta ya viwanda.

China pia imeahidi kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Hayo yameelezwa Rais Xi Jinping wa China wakati wa mazungumzo yake na Rais Samia Suluhu Hassan, mazungumzo yaliyofanyika kwa njia ya simu.

Wakati wa mazungumzo yao, Viongozi hao wamekubaliana kukuza ushirikiano katika nyanja za uchumi, utamaduni na ushirikiano wa Kimataifa.

Rais Xi Jinping amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua kijiti cha uongozi, na kumpa pole kutokana na kifo cha Rais wa awamu ya tano Dkt. John Magufuli.

Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan ametumia mazungumzo hayo kutoa salamu za pongezi kwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kwa kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, na ameahidi kudumisha uhusiano kati ya chama hicho na Chama Cha Mapinduzi (CCM).