Sabaya na wenzake ngoma nzito

0
251

Aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne kwa mara nyingine wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi ikiwemo na utakatishaji fedha namba 27 ya mwaka 2021 imetajwa na Wakili Mkuu wa Serikali Msaidizi Abdallah Chavula mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Martha Mahumbuga.

Wakili Abdallah Chavula amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa tena.

Kwa Upande wa utetezi unaowakilishwa na Wakili Moses Mauna, umeiomba mahakama hiyo kuharakisha upelelezi wa shauri hilo huku ukiomba pia kupatiwa hati ya kesi hiyo.

Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 2 mwaka huu itakapotajwa.

Aidha katika hatua nyingine kesi ya jinai namba 66 ya mwaka 2021 ambayo ni ya unyang’anyi wa kutumia silaha yenye mashtaka mawili inayowakabili washtakiwa Lengai Ole Sabaya na wenzake imetajwa katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi Salome Mshasha.

Katika kesi ya msingi wakili wa Serikali Tarcila Gervas amesema kuwa Februari 9 mwaka huu Sabaya na wenzake Sylvester Nyegu na Daniel Mbula wanadaiwa kufika kwenye duka la Saad lililopo mtaa wa Bondeni Arusha na kuwaamuru Wafanyakazi wa duka hilo kulala chini huku wakiwapiga na kuwanyooshea bunduki na kuwatishia kuwafyatulia risasi.

Katika shauri hilo mmoja wa watuhumiwa anadaiwa kumfunga kamba diwani wa kata ya Sombetini Bakati Msangi na kuchukua zaidi ya Shilingi laki tatu na simu moja aina ya Tekno na shilingi elfu 35 kutoka kwa Ramadhan Rashid.

Watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti na kukiri kuwepo kwenye duka hilo huku wakikana kutenda kosa hilo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai mbili mwaka huu itakapotajwa tena.