Rais : Dkt. Kaunda alikuwa mahiri na jasiri

0
208

Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Rais Edgar Lungu wa Zambia, familia ya marehemu  na wananchi wote wa Zambia kufuatia kifo cha Rais wa kwanza wa Taifa hilo Dkt. Kenneth Kaunda kilichotokea hapo jana mjini Lusaka.

Katika salamu zake, Rais Samia Suluhu Hassan amemtaja Hayati Dkt. Kaunda kuwa ni miongoni mwa viongozi mahiri na jasiri kuwahi kutokea Barani Afrika.

Amesema wakati wa uhai wake Dkt. Kaunda alitoa mchango mkubwa kwenye harakati za ukombozi wa bara hilo kwa kushirikiana na viongozi wengine, akiwemo Baba wa Taifa la Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza kuwa Hayati Dkt. Kaunda alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). 

Amesema Tanzania itamkumbuka Hayati Dkt. Kaunda kwa mchango wake katika kukuza uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa yetu mawili, ambao uliwezesha kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Mamlaka ya Reli kati ya Tanzania na Zambia (TAZARA) na Bomba la Kusafirisha Mafuta (TAZAMA).